Hatimaye Bunge la Kitaifa limepitisha kwa kauli moja, Mswada wa Marekebisho ya Katiba wa Mwaka 2025, unaonuia kujumuisha kwenye katiba hazina ya serikali ya kitaifa ya ustawi wa maeneo bunge NG-CDF, hazina ya serikali ya kitaifa inayotengewa makundi maalum, NGAAF na hazina ya usimamizi ya Bunge la Seneti, SOF.
Wakati mswada huo uliposomwa kwa mara ya pili bungeni, wabunge 304 walipiga kura kuunga mkono – hakuna yeyote aliyeipinga. Wakati iliposomwa mara ya tatu, wabunge wote waliunga mkono mswada huo uliowasilishwa bungeni kwa pamoja na mbunge wa Rarieda Otiende Amollo na Samuel Chepkonga wa Ainabkoi Machi 12,2025.
Kamati ya Haki na Maswala ya Katiba ilikua imepokea mswada huo ili kuufanyia ukarabati, na kukusanya maoni ya umma katika maeneo bunge yote 290 na kuwasilisha ripoti yake Juni 17,2025, ikidokeza kuwa asilimia 98 ya waliotoa maoni, waliunga mkono hazina hiyo.
Hazina ya NG-CDF, kulingana na Kinara wa waliowengi Bungeni Mbunge wa Kikuyu Kimani Icu’ngwa na mwenzake wa walio wachache Mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohammed, inanuia kuhakikisha upatikanaji sawa wa huduma za serikali ya kitaifa hasa elimu na muundomsingi katika kiwango cha mashinani.
“Bwana Spika, naunga mkono NG-CDF maana inanuai kusaidia serikali za kaunti kuboresha huduma kwa raia mashinani,” alisema Icu’ngwa, Jumanne.
“…naunga mkono mswada wa NG-CDF Bwana Spika na naomba wenzetu maseneta kwenye bunge la Seneti kuunga mkono NG-CDF pia,” aliongeza Junet.
Kwa upande mwingine, hazina ya SOF inalenga kuimarisha jukumu la usimamizi wa Seneti kwa serikali za kaunti huku ile ya NGAAF ikiimarisha ufadhili kwa makundi yasiyojiweza wakiwemo wanawake, vijana na wnaoishi na ulemavu.
Bunge la seneti linatarajiwa kupokea mswada huo ili kuujadili na kuamua ikiwa litaunga mkono mapendekezo ya bunge la kitaifa au la, kabla ya Rais William Ruto kutia saini.