Huku zikiwa zimesalia siku za kuhesabu kabla Jumatatu ya Sabasaba (Julai 7, 2025) siku ambayo vijana wa Gen Z wametangaza maandamano ya kitaifa dhidi ya serikali ya Rais William Ruto, wasiwasi unaendelea kuwakumba wafanyibiashara sehemu mbalimbali, kwa hofu ya biashara zao kuvamiwa na waporaji wanao-ingilia maandamano hayo kwa nia mbaya.

Katika eneo-bunge la Mavoko kaunti ya Machakos, wakazi wa Athi River wanapinga mikutano ya hadhara ya kuadhimisha siku hiyo.

Kundi la wakazi wanaoshirikiana na chama tawala cha UDA limelalamika kwamba maandamano yaliyopita ya kupinga serikali yaliingiliwa na wahuni na kuacha uharibifu mkubwa na wizi ambao unahatarisha usalama wa taifa.

Kulingana nao, tukio la Saba Saba la mwaka wa 1990 ni kumbukumbu muhimu ya demokrasia ya vyama vingi na utawala bora nchini, lakini kwa hali ya sasa ya maandamano nchini, chuki na ghadhabu vimetawala taifa, jambo ambalo ni mwiko kugusa.

Katika kaunti ya Mombasa, kundi moja la wanawake limejitokeza kuwarai vijana kutoshiriki maandamano, ikiwemo inayotarajiwa Jumatatu juma lijalo ‘Maandamano Ya Saba Saba’.

Kundi hilo likiongozwa naye Warda Ahmed na Afia Rahma, limesema maandamano hayo yamegeuka kuwa hasara kubwa inayohatarisha amani ya taifa.

“Tunawarai watoto wetu kusikiliza na kuipa serikali muda wa kufanya kazi. Tusiharibu nchi yetu kwa maandamano. Kenya ni moja hakuna haja ya kuiharibu,” alisema Ahmed.

Waziri wa Kilimo Mutahi Kagwe ameonya wote wenye nia ya kutumia maandamano ya amani kuzua ghasia na kuendeleza uporaji, juma moja baada ya ghala la NCPB, Maua, kaunti ya Meru kuvamiwa na jumla ya mifuko zaidi ya alfu saba ya mbolea kuibwa.

“Wanaovamia maduka na majengo na kuiba mali ya umma na ya kibinafsi ni wezi, wala siyo waandamanaji vijana wa Gen Z, na wanapaswa kukabiliwa vilivyo kisheria,” Kagwe alisema.

Waziri huyo alizungumza akiwa katika ghala la NCPB kaunti ya Nakuru, baada ya kuhudhuria maonyesho ya kilimo ya kila mwaka ya ASK, kaunti ya Nakuru.

Kwingineko ni kuwa wahudumu wa afya humu nchini wametishia kususia kutoa huduma zao iwapo watazidi kuwekwa hatarini wakati wa maandamano.

Wakiongozwa na Katibu wa chama cha KMPDU Davji Atellah na Katibu wa KUCO George Gibore, wamekosoa maafisa wa polisi wakisema wanafanya kazi na wahuni wanaoingilia maandamano kuhangaisha maafisa wa afya wanaotoa msaada wa afya kwa waandamanaji wanaoumia wakati wa maandamano, na wanapoelekea makazini pia.

“Tunahitaji mwelekeo wa mazungumzo kuhusu masuala yanayotusibu kama taifa. Hii tabia ya uharibifu na madhara kwa raia na wahudumu wa afya haikubaliki. Polisi wanapaswa kujizuia, raia pia,” Davji alisisitiza katika mkutano na wanahabari jijini Nairobi.