Mwalimu mmoja kutoka Shule ya Msingi Mikindani, eneo bunge la Jomvu, Kaunti ya Mombasa, amefariki dunia kufuatia ajali mbaya ya barabarani iliyotokea jioni ya Alhamisi, eneo la Maasai, Taita Taveta, kwenye barabara kuu ya Mombasa – Nairobi.

Mwalimu huyo alikuwa akiandamana na wanafunzi waliokuwa wakirejea kutoka Shule ya Upili ya Kenyatta, ambako walishiriki katika tamasha ya muziki na maigizo, kanda ya pwani.

Katika ajali hiyo, wanafunzi wawili walijeruhiwa vibaya, huku wengine 10 wakipata majeraha madogo, wote, wakifikishwa katika Hospitali ya Mikindani Medical kwa ajili ya matibabu.

Mbunge wa Jomvu, Badi Twalib, alitembelea Shule ya Msingi ya Mikindani Comprehensive, kufuatilia hali ya wanafunzi na kuwapa faraja waliokua wakipokea matibabu.

Twalib akizungumza na wazazi ambao walifika shuleni humo Alhamisi usiku kutafuta uhalisia wa hali na hali ya watoto hao, ambao walikua wakitumia basi la Shule ya Upili ya Kajembe kwa safari hiyo wakati wa ajali, alisema, “kama mjumbe wenu, pia mimi ni mzazi. Nililipa bili ya hospitali ya wanafunzi hao Mikindani Medical Hospital na wanafunzi hao wakaruhusiwa kuenda nyumbani.”

Huku akisikitikia kifo cha mwalimu wa shule hiyo, mbunge huyo aliwahakikishia wazazi kuwa watoto wao walikua salama na kwamba atahakikisha wanapata ushauri nasaha na kuangaliwa kimatibabu vyema, kwa ushirikiano na ofisi ya Mkurugenzi wa elimu, kaunti ndogo ya Jomvu, Bi. Maimuna.