Mabingwa mara mbili wa kombe la Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN), DR Congo, maarufu kama the Leopards (Chui), waliwasili nchini mapema Alhamisi kupitia uwanja wa JKIA tayari kushiriki kipute cha mwaka huu ambacho kitaendelea nchini Kenya, Uganda na Tanzania.

Chui wa DR Congo wamekuwa kwenye kambi ya mazoezi jijini Dar es Salaam, Tanzania, tangu mwishoni mwa wiki jana kujiandaa kwa kipute cha CHAN wakijiuvunia kutawazwa mabingwa mwaka 2009 na 2016, na sasa wanamezea mate kombe la CHAN2024.

Vijana hao wanatarajiwa kufungua mechi za kundi A Jumapili hii ya Agosti 2, 2025 dhidi ya wenyeji Harambee Stars ya Kenya katika uwanja wa Kasarani, jijini Nairobi saa 3:00pm saa za Afrika Mashariki.

Timu nyingine kundini A ni Congo, Morocco, Angola, na Zambia, Kenya wakihitajika kujikakamua ili kuondoka kundini na ushindi.

Harambee Stars itashiriki fainali za CHAN kuanzia tarehe 2 hadi 30 Agosti bila huduma za wachezaji nyota wa Ligi Kuu msimu uliomalizika.

Kocha mkuu wa Harambee Stars Benni McCarthy, raia wa Afrika Kusini, amelazimika kuwaita kambini wanandinga wengine baada ya kiungo mkabaji Mohammed Bajaber wa Police FC kuondoka kikosini Jumatatu, kujiunga na miamba wa Tanzania Simba, walio kambini nchini Misri.

Bejaber mwenye umri wa miaka 22, amesaini mkataba wa miaka mwili na wekundu wa msimbazi Simba.

Harambee Stars pia itazikosa huduma za mfungaji bora wa ligi kuu msimu jana, Moses Shumah wa Kakamega Homeboyz, ambaye amejiunga na klabu ya Power Dynamos ya Zambia.

Shumah aliongoza chati ya ufungaji mabao katika ligi kuu ya Kenya msimu wa mwaka 2024/2025, kwa jumla yaa magoli 17.

Aidha, mfungajii bora wa pili Emmanuel Osoro wa Talanta FC, aliyepachika mabao16 msimu jana, alijiondoa kikosini baada ya kusainiwa na Dynamos ya Zambia kwa kandarasi ya miaka miwili.