Shule ya Upili ya Wasichana ya St. George’s, iliyoko Kilimani, jijini Nairobi, imefungwa kwa muda usiojulikana baada ya usiku wa vurughu na mvutano mkali kati ya wanafunzi na walimu.
Ghasia zilizowahusisha wanafunzi zaidi ya 1,800 zilianza jana Jumapili Septemba 7, usiku kufuatia madai ya kisa cha kugombana kati ya mwalimu na mwanafunzi wa Kidato cha tatu, majira ya saa tatu na nusu usiku, tukio linalodaiwa kumwacha mwanafunzi huyo na jeraha mdomoni.
Tukio hilo lilizua ghadhabu miongoni mwa wanafunzi, ambao walivunja lango la shule na kuandamana na kisha kupiga kambi katika barabara jirani ya Dennis Pritt wakidai kunyanyaswa na walimu shuleni. Polisi walifika karibu saa sita usiku na kuwarejesha wanafunzi ndani ya shule, ingawa walikataa kurejea katika mabweni yao.
Kufikia Jumatatu asubuhi, mvutano huo ulikuwa umevutia maafisa wa serikali na elimu, wakiwemo Kamishna wa Kaunti Ndogo ya Dagoretti Kaskazini, maafisa kutoka Wizara ya Elimu, na OCPD wa Kilimani, Patricia Yegon, waliokuwa wakijaribu kutuliza hali.

Majira ya saa nne asubuhi, uongozi wa shule ulitangaza kufungwa kwa shule hiyo kwa muda usiojulikana, na kuwapa wanafunzi muda wa dakika 20 tu kuondoka shuleni. Wakati huo, baadhi ya wazazi tayari walikuwa wamewasili kufuatia taarifa hiyo.
Baadhi ya wanafunzi walilazimisha kufungua lango, huku wengine wakitembea kwa makundi, wakiimba na kuwazuia madereva barabarani. Wakazi waliokuwa wamepigwa na butwaa walitazama maandamano hayo yakiendelea hadi usiku wa manane.
Wazazi waliowasili shuleni mapema Jumatatu asubuhi walikuta maafisa wakiwa walinzi katika lango, huku walimu na wasimamizi wakishiriki mazungumzo yenye mvutano.
Wanafunzi kadhaa walionekana wakibeba mizigo yao kwa matarajio ya kufungwa kwa shule hata kabla ya tangazo rasmi kutolewa.
“Tuliamshwa kwa kelele na vurughu,” alisema mkazi mmoja wa Kilimani, akiongeza kuwa hali iligeuka haraka na kuwa machafuko. “Ilikuwa dhahiri watoto walidhamiria kutorudi darasani.”
Mkuu wa Kaunti Ndogo ya Dagoretti Kaskazini, Juma, na OCPD wa Kilimani Yegon baadaye walithibitisha kuwa serikali imeamua kuwatuma wanafunzi manyumbani.
“Usalama wa wanafunzi ni jambo la kwanza. Shule itasalia kufungwa hadi taarifa itakapotolewa tena, na wazazi watajulishwa hatua zitakazofuata,” Juma alisema baada ya kikao na bodi pamoja na walimu.
Wazazi walipokea uamuzi huo kwa furaha, wengi wakieleza afueni kwamba hakuna mwanafunzi aliyejeruhiwa wakati wa machafuko hayo ya usiku.