Serikali ya kitaifa na magavana wa kaunti wamekubaliana kuharakisha kupanga upya miradi ya kilimo inayofadhiliwa na Benki ya Dunia ili kukabiliana na ukame unaoikumba Kenya huku wakijenga uthabiti wa muda mrefu.

Akizungumza baada ya mkutano wa ngazi ya juu uliofanyika Malindi Kaunti ya Kilifi na Kamati ya Kilimo ya Baraza la Magavana pamoja na Jopo la Magavana wa maeneo kame na nusu-kame (ASAL), Waziri wa Kilimo Mutahi Kagwe alisema “juhudi hizo zitachukua mkabala wa serikali nzima, kwa kuangalia mazao, mifugo na maisha ya wananchi kama mfumo mmoja unaounganishwa.”

“Majadiliano yalilenga Mpango wa Ustahimilivu wa Mifumo ya Chakula (Food Systems Resilience Program – FSRP), unaotekelezwa katika kaunti 13 zilizoathirika zaidi, pamoja na Mradi wa Kitaifa wa Maendeleo ya Minyororo ya Thamani ya Kilimo (National Agricultural Value Chain Development Project – NAVCDP), unaotekelezwa katika kaunti 34 zilizosalia.”

Fedha zitaelekezwa upya kusaidia hatua za dharura za kukabiliana na ukame, ikiwemo usafirishaji wa malisho, usambazaji wa maji na ulinzi wa mifugo, huku baadhi ya shughuli zilizopangwa awali zikisitishwa kwa muda.

Viongozi, kwenye mkutano huo, walikubaliana kuwa angalau asilimia 85 ya rasilimali zitaelekezwa moja kwa moja kwenye utekelezaji mashinani, huku kaunti zikipewa jukumu kuu katika upangaji na utekelezaji wa miradi.

Mkakati huo pia unaweka kipaumbele umwagiliaji, hifadhi za malisho, udhibiti wa magonjwa, mifumo ya kilimo kidijitali, na ushirikishwaji wa vijana, ili kupunguza utegemezi wa kilimo cha kutegemea mvua na kujiandaa kwa misukosuko ya tabianchi siku zijazo.