Chama cha Pamoja African Alliance (PAA) kinachoongozwa naye Spika wa Bunge la Seneti Amason Kingi, baada ya kuwa Gavana wa Kilifi chini ya chama cha ODM, kwa miaka kumi – kutoka 2013 – 2022, sasa kimezama.
Kingi ametangaza chama hicho kimevunjwa ili kuungana na chama tawala cha UDA anachoongoza Rais William Ruto, kwa matayarisho ya uchaguzi wa 2027.

Hivyo basi hakitaweka wagombea wa kisiasa eneo lolote nchini, na badala yake, kitakua kinauza sera za UDA, kama tu kile cha ANC, alichoongoza Musalia Mudavadi, ambaye sasa ni Mkuu wa Mawaziri, na Waziri wa Maswala ya Kigeni.

“Tumekua na mazungumzo kwa muda mrefu na rais, na baada ya mazungumzo hayo, tumekubaliana kuwa chama cha Pamoja African Alliance hakitakua na wagombea kwenye uchaguzi ujao. Badala yake, tutaunga mkono chama cha UDA,” Kingi alisema akiwa eneo la Swahili Pot, Mombasa.

Chama cha PAA kimekua na umaarufu zaidi ukanda wa Pwani, hasa Kilifi, Mombasa, Kwale na Lamu na kilitarajiwa kuvuna pakubwa katika uchaguzi wa 2027.