Kongamano la wajumbe wa chama cha ODM (NDC) linalotarajiwa kufanyika mnamo Machi 27, 2026 limegeuka kuwa jukwaa la vuta n’kuvute na mkwaruzano wa vita vya kisheria na kutishia kuyumbisha chama hicho baada ya kifo cha mwanzilishi wake, Raila Odinga.
Mbunge wa Saboti Caleb Amisi anasema yeye pamoja na wenzake katika mrengo wa ‘Linda Mwananchi hawatahudhuria kongamano hilo.
Kulingana na Caleb Amisi, NDC inayotarajiwa Machi 27 inakiuka katiba ya chama, akisisitiza kuwa ni lazima uitishwe rasmi na Katibu Mkuu Edwin Sifuna kufuatia uamuzi wa mahakama uliomrejesha mamlakani, baada ya kutemwa na vinara wa chama.
“NDC inafaa iitwe na Sifuna. Ile NDC haijaitwa na Sifuna ni ya wakora, na Baba (Raila) hajafurahia mahali yuko…” Amisi alisema akiwa katika Knaisa la Full Gospel, Kapretwa, Saboti.
Usemi wake unaendana na wa Kampuni ya Uwakili inayowakilisha mwanachama wa ODM Vincent Chepkwony ambaye amezua maswali kuhusu uhalali wa kisheria wa kongamano hilo, akidai kuwa notisi ya kuandaliwa kwa NDC ilitolewa na Naibu Katibu Mkuu – Catherine Omanyo, badala ya katibu mkuu – Edwin Sifuna, jinsi ambavyo imenakiliwa kwenye Katiba ya ODM.
Kifungu cha 49 cha Katiba ya ODM kinasema kuwa Kongamano Spesheli la Wajumbe wa chama litaitishwa na Mwenyekiti kupitia uamuzi wa Kamati ya Kitaifa ya Chama au kupitia ombi la theluthi moja ya wajumbe wanaostahili kuhudhuria mkutano huo.
Katiba hiyo hiyo inasema notisi na ajenda ya mkutano huo itatumwa na Katibu Mkuu zaidi ya siku 21 kabla ya tarehe hiyo na pia kuchapishwa katika mtandao wa chama.
Aidha, notisi na ajenda hiyo lazima ichapishwe katika gazeti moja la Kingereza au idhaa moja ya Kiswahili.
Chepkwony pia amezua maswali kuhusu uhalali wa kisheria wa orodha ya wajumbe ambao wanatarajiwa kuhudhuria kongamano hilo, kwani kaunti nne ambazo ni Migori, Kisumu, Nairobi na Taita Taveta bado hazijaandaa chaguzi ndogo za mashinani.
Wakati huo huo, vuguvugu la ODM, linaloongozwa na Katibu Mkuu ambaye pia ni Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna baada ya kuweka breki kwa muda, mikutano yao ya kisiasa, wametangaza upya kuziendeleza.
Sifuna, kupitia mitandao ya kijamii, ametangaza kuwa baada ya mkutano wa mwisho kaunti ya Kakamega mwezi uliopita, wamerejea upya na kwamba Jumapili ya Machi 22, wataandaa mkutano wa Linda Mwananchi mjini Narok, kisha kaunti ya Nairobi – Ijumaa ya Machi 27 siku ya NDC ya ODM, na kisha Jumapili ya Machi 29, jijini Mombasa.
Kulingana na kundi hilo ambalo Amisi ni mfuasi, watafanya kikao na wananchi kama NDC mbadala Machi 27 jijini Nairobi.
Sifuna na kundi lake wanapoendeleza kampeni hizo na kuwataka wakenya wajisajili na vuguvugu hilo kupitia mtandaoni, Seneta wa Nandi Samson Cherargei ameendelea kumlaumu Rais mstaafu Uhuru Kenyatta, akidai kuwa ndiye anayetoa fedha za kufadhili vuguvugu hilo, ili kufanya uongozi wake Rais William Ruto kuyumba.