Shirikisho la Soka Barani Afrika (“CAF”) kupitia Kamati yake ya Nidhamu limekutana kujadili masuala mbalimbali yanayohusiana na Mashindano ya Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (“CHAN”) PAMOJA 2024 yanayoendelea Kenya, Uganda na Tanzania, chini ya udhamini wa TotalEnergies.

Shirikisho la Kandanda Nchini Kenya (FKF), limepigwa faini ya shilingi milioni 6.5 ambazo ni Dola za Marekani 50,000  kutokana na visa vya utovu wa usalama wakati wa mechi baina ya Kenya na Morocco, kuwania kombe la CHAN Jumapili iliyopita katika uwanja wa kimataifa wa Kasarani.

Kamati ya nidhamu ya shirikisho la soka barani CAF imeitoza FKF faini hiyo baada ya baadhi ya mashabiki kuvunja lango la kuingia Kasarani na polisi kushindwa kuthibiti umati.

Kamati ya Nidhamu ya CAF ililishitaki Shirikisho la Soka la Kenya (“FKF”) kwa kukiuka masharti ya usalama na ulinzi mara kadhaa wakati wa mechi ya CHAN kati ya Kenya na Morocco iliyofanyika katika Uwanja wa Kimataifa wa Moi, Kasarani.

Kenya ilipewa onyo kuwa iwapo itaendelea kushindwa kutimiza mahitaji ya usalama na ulinzi ya CAF, mechi za timu ya taifa ya Kenya zinaweza kuhamishiwa kwenye uwanja mbadala.

Kenya ilishauriwa kuimarisha hatua za usalama kwa kuongeza idadi ya askari na maafisa wa ulinzi kuzunguka uwanja, pamoja na kufuata masharti ya kufunga barabara siku za mechi.

FKF imewataka mashabiki wa Kenya kutilia maanani kanuni za CAF katika mpira wa miguu ili kuiweka Kenya salama kwa mechi zijazo.

Mchuano wa mwisho ya kundi A kuwania kombe la CHAN kati ya Kenya na Zambia, Jumapili hii uwanjani Kasarani, umerejeshwa nyuma kutoka saa mbili usiku hadi saa tisa alasiri.

Mchuano huo utachezwa sambamba na ule kati ya DR Congo na Morocco katika uwanja wa Nyayo.

Hata hivyo, ni idadi ndogo ya mashabiki watakaofika uwanjani Kasarani baada ya CAF kupunguza idadi ya tiketi kutoka 48,000 hadi 27,000 kutokana na matatizo ya kiusalama ambayo yameshuhudiwa katika mechi zilizopita za CHAN. Tayari tiketi za mechi hiyo zimetamatika, masaa masita baada ya tuvuti ya kuzinunua kufunguliwa.

Kenya ni sharti waishinde Zambia ili kujihakikishia nafasi ya kwanza kundini humo na kuwa mwenyeji wa mechi ya robo fainali.

Rais Ruto amewaahidi wachezaji wa timu ya taifa ya soka ya Kenya Harambee Stars shilingi milioni 2.5 kila mmoja endapo wataishinda Zambia Jumapili Agosti 17, katika mechi ya mwisho ya kundi A kuwania kombe la CHAN.

Aidha, Ruto ameahidi kuwa endapo Kenya watashinda mechi ya robo fainali, kila mchezaji atapata nyumba ya vyumba viwili chini ya mpango wa nyumba za gharama nafuu mahali watakapochagua pamoja na kitita cha shilingi milioni 1 kila mmoja.

Kadhalika, Kamati ya Nidhamu ya CAF ililishitaki Shirikisho la Soka la Zambia (“FAZ”) kwa kukiuka Kanuni za Vyombo vya Habari za CAF wakati wa mkutano wa wanahabari wa Siku ya Mechi ya Kwanza, kabla ya mechi yao ya CHAN dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Zambia ilishindwa kumwasilisha kocha mkuu katika mkutano huo wa lazima wa wanahabari. Kamati ya Nidhamu ililipata kosa na kuliwekea faini ya Dola za Marekani 5,000.

Kwenye mkutano huo, Kamati ya Nidhamu ya CAF pia ililishitaki Shirikisho la Soka la Ufalme wa Morocco (“FRMF”) kwa tabia isiyofaa ya wachezaji wake wakati wa mechi ya CHAN kati ya Morocco na Kenya.

Kamati ya Nidhamu ililipata Morocco na kosa na kuliwekea faini ya Dola za Marekani 5,000, ambapo Dola za Marekani 2,500 zimeahirishwa kwa masharti kwamba kosa kama hilo lisitokee tena katika kipindi kilichosalia cha CHAN 2024.

Faini zote zinapaswa kulipwa ndani ya siku 60 tangu tarehe ya taarifa ya uamuzi huu.