Msimu huu wa Sikukuu ya Krsimasi, Gavana wa Kaunti ya Machakos, Wavinya Ndeti, amewataka madereva kuwa waangalifu zaidi barabarani.

Akizungumza baada ya kuhudhuria hafla ya ubatizo wa watoto katika Kanisa la Our Lady of Lourdes mjini Machakos, Gavana Wavinya alionya dhidi ya uendeshaji usiozingatia sheria, mwendo wa kasi kupita kiasi, akisema vitendo hivyo vimechangia kuongezeka kwa ajali za barabarani.

Aliwahimiza madereva kuepuka kuendesha magar wakwia walevi akishauri familia kuhakikisha kutotumia dereva mlevi wakati wa sherehe za sikukuu.


“Madereva waache kuendesha gari wakiwa walevi ili kuepuka kuhusika katika ajali za barabarani krisimasi hii,” alisema Ndeti.
 
Hayo yanajiri wakati ambapo ndugu wawili na mchungaji wa mifugo ni miongoni mwa watu wanne waliofariki katika ajali ya barabarani iliyotokea usiku wa Jumatano, kwenye barabara kuu ya Namanga, kaunti ya Kajiado.

Ajali hiyo iliyotokea mwendo wa saa tisa usiku ilihusisha pikipiki na lori karibu na mahakama ya Kajiado, huku mhudumu wa pikipiki na abiria wake watatu wakifariki papo hapo. Waathiriwa waliokuwa wakitoka kwenye jumba la burudani walikuwa na umri wa kati ya miaka 40-47.

Kulingana na ripoti ya polisi, lori hilo lililokuwa likielekea mji wa Kajiado lilikuwa likiendeshwa kwa kasi.

Miili ya waathiriwa ilipelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya Rufaa ya Kajiado na mabaki ya lori na pikipiki kuvutwa hadi kituo cha Polisi cha Kajiado.

Katika muda wa wiki moja, jumla ya watu sita wamefariki katika ajali tofauti za barabarani katika barabara kuu ya Namanga, wengine wengi wakijeruhiwa.

Katika juhudi za kupunguza ajali Kaunti ya Laikipia, Mamlaka ya Kitaifa ya Usafiri na Usalama Barabarani (NTSA) kwa ushirikiano na idara ya polisi wa trafiki mjini Nanyuki kaunti ya Laikipia, imezindua kampeni ya uhamasishaji.

Kampeni hiyo, inayoungwa mkono na shirika la kijamii eneo hilo kwa jina Binti Mwangaza, pamoja na afisa kutoka Jeshi la Uingereza, inajumuisha mafunzo ya usalama barabarani na ugawaji wa majaketi ya viakisi mwanga kwa vijana wanaotembea kwa miguu na wanaboda boda ili kuongeza usalama wao barabarani.

Kwa mujibu wa waandalizi wa kampeni hiyo, huu ni mpango wa muda mrefu ambao utatekelezwa katika shule za msingi zitakapofunguliwa mwezi ujao, kwa lengo la kuhakikisha usalama wa wanafunzi wanapotumia barabara zenye msongamano mkubwa wa magari.

Madereva na wanaotembea kwa miguu wamehimizwa kuzingatia sheria za trafiki na kudumisha nidhamu barabarani ili kuepuka ajali na vifo zaidi.


Kwa mujibu wa takwimu za serikali, wanaotembea kwa miguu, waendesha baiskeli na boda boda ndio wanaochangia kwa kiwango kikubwa ajali hatari za barabarani nchini.

Kuanzia Januari hadi Machi mwaka huu, vifo vya wanaotembea kwa miguu vilikuwa vingi zaidi, vikiwa 420 kati ya vifo 1,139 vilivyosababishwa na ajali za barabarani.

Takwimu za NTSA zinaonyesha kuwa ajali za barabarani zimeongezeka hadi 4,682 mwaka huu ikilinganishwa na 4,479 mwaka jana, hali iliyochangia kuundwa kwa kamati ya kitaifa ya mashirika mbalimbali kushughulikia mwenendo huo.