Timu ya taifa ya Algeria, maarufu kama ‘The Dessert Foxes’, waliwatoa kijasho wenzao wa Uganda, maarufu kama ‘Uganda Cranes’ na kuwapa kichapo cha mbwa katika mechi ya kundi C.
Mbweha hao waliwachachafya Korongo mabao 3-0, kuwania kombe la CHAN, iliyosakatwa Jumatatu saa mbili usiku kiwanjani Mandela jijini Kampala, Uganda.
Algeria walianza kwa matao ya juu wakichukua uongozi katika dakika ya 36, kupitia kwa nahodha Ayoub Ghezala, aliyeunganisha pasi ya Abderrahmane Meziane kwa kichwa.
Katika kipindi cha pili, maji yalizidi unga kwa Korongo, baada ya Mbweha kuwamiminia magoli mawili ya haraka ndani ya dakika tatu. Meziane na Soufiane Bayazid waliutia mpira kwenye wavu dakika za 76 na 79 mtawalia.
Sasa itawabidi Waganda kujipanga upya kwa mchuano wa pili dhidi ya Guinea, mnamo Agosti 8. Hawana budi kushinda ili kuweka hai matumaini ya kufuzu kwa robo fainali kwa mara ya kwanza.
Kwenye mechi ya kwanza ya kundi C, uwanjani humo, Guinea waliwazabua Niger bao moja kwa nunge.
Uganda ni wenyeji wenza wa mchuano wa CHAN, pamoja na Tanzania na Kenya, ambao walishinda mechi yao ya kwanza dhidi ya Burkina Faso na DR Congo mtawalia, kwa mabao 2-0 na 1-0.