Usafiri wa matatu jijini Nairobi umeathirika vibaya Jumatatu hii, baada ya baadhi ya madereva na wamiliki wa magari ya usafiri wa umma (matatu) kuanza mgomo, licha ya taarifa ya kusitishwa kwa hatua hiyo iliyotolewa Jumapili. 
 
Barabara kuu na maeneo mengine yamekumbwa na msongamano mkubwa wa magari huku abiria wengi wakibaki bila usafiri, wengine wakilazimika kutembea kwa miguu.
Image

Katika maeneo kama Outering Road karibu na Kariobangi Roundabout, madereva walizuia barabara kwa kuegesha magari yao katikati ya barabara, hali ambayo ilizifanya barabara ya Outering Road na Thika Road kuvurugika.

“Tumeamka mapema sana, lakini hakuna matatu yoyote. Sijui nitakaje kazini,” alisema abiria mmoja katika kituo kimoja cha magari, barabara ya Tom Mboya.

Wakati huo huo, baadhi ya wamiliki wa matatu wakiongozwa na Albert Karakacha wameeleza kuwa mgomo huo ni njia ya kulazimisha serikali kushughulikia tatizo la ukosefu wa usalama barabarani, hasa baada ya matatu kadhaa kuchomwa moto bila hatua madhubuti kuchukuliwa dhidi ya wahalifu wanaosababisha madhara hayo, kila mara wakati gari linapohusika kwenye ajali na pikipiki za usafiri wa umma aina ya ‘bodaboda’.

Aidha, uwepo kwa askari barabarani wanaojaribu kudhibiti msongamano na kuongoza usafiri kwa magari binafsi, umeonekana sehemu mbalimbali kama Westlands na katikati mwa jiji, waendesha pikipiki za bodaboda wakivuna pakubwa kwa kuwasafirisha abiria waliokwama, kwa ada kubwa, huku wamiliki wa matatu wakisema wana mipango ya kuendelea na mgomo kila Jumatatu hadi serikali ichukue hatua dhidi ya uhalifu dhidi ya magari barabarani.


Abiria wametakiwa kutumia njia mbadala za usafiri na kupanga safari mapema kutokana na hali hiyo isiyotabirika barabarani.