Mwanablogu aliyekuwa ametoweka Ndiangui Kinyagia amejitokeza katika mahakama kuu Jijini Nairobi Alhamisi Julai 3, 2025, baada ya mahakama hiyo kuagiza mkuu wa idara ya upelelezi wa jinai Mohamed Amin, kumwasilisha.

Kinyagia alitoweka akiwa katiak nyumba yake ya kukodi, mtaani Kinoo, kaunti ya Kiambu Juni 22, 2025 baada ya kile ambacho majirani walitaja kuwa kilikua ni uvamizi wa maafisa wa upelelezi wa jinai nyumbani kwake.

Alhamisi alfajiri, wakili wa familia Wahome Thuku alitangaza kwamba alikuwa amewasiliana na familia yake, akawafahamaisha kwamba yuko salama na akaahidi kufika mahakamani.

Thuku alisema “Ndiangui aliwasiliana na mmoja wa watu wa familia yake Jumanne jioni kutoka eneo lisilojulikana na kumueleza alikuwa amejificha baada ya kufahamu maafisa wa upelelezi walikuwa wakimtafuta.”

Awali idara ya upelelezi wa jinai kupitia mkurugenzi wake Amin, ilikuwa imekanusha kumshikilia mwanablogu huyo, mahakama kuu nayo Jumatatu juma hili ikitoa agizo kwa Inspekta Jenerali wa polisi Douglas Kanja, amuwasilishe Kinyagia mahakamani Jumanne juma hili asubuhi au aelezee aliko.

Kupatikana kwake ni afueni kwa familia yake ikiongozwa na mamake Lilian Wanjiku, ambayo iliandamana naye mpaka mahakamani Alhamisi hii mawakili wake wakisema alikua mnyonge na mwenye hofu, na kuitaka Mahakama chini ya Jaji Chacha Mwita kumruhusu aende nyumbani atangamane na familia yake.

Mahakama pia ilizuia Idara ya Usalama kumkamata mwanablogu huyo, jambo ambalo mahakama iliridhia. Wakili na Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino amekua msitari wa mbele kutafuta haki kwa Kinyagia mahakamani, huku akiikosoa idara ya DCI.

Kesi hiyo itasikilizwa tena Julai 18, mwaka huu.