Idadi ya watu waliofariki kufuatia mafuriko yanayoshuhudiwa nchini imefikia 71 baada ya watu watano zaidi kufariki katika kaunti ya Nairobi, ukanda wa Mashariki na Mkoa wa Pwani.

Haya yanajiri wakati idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa nchini Kenya ikionya kuwa mvua itaongezeka kuanzia Alhamisi ya kesho (Machi 19, 2026), katika maeneo kadhaa ya nchi huku msimu wa mvua ndefu ukianza kushika kasi.

Katika utabiri wake wa hali ya hewa wa kila wiki, kuanzia Machi 17 hadi Machi 23, 2026 uliotolewa Jumatatu, Machi 16, 2026, idara hiyo ilisema mvua itaendelea kunyesha katika maeneo mengi, mvua kubwa ikitarajiwa mwishoni mwa wiki.

Mvua hiyo “itaathiri zaidi maeneo matano nchini, ikijumuisha Nyanda za Juu Mashariki na Magharibi mwa Bonde la Ufa, Bonde la Ziwa Victoria, Bonde la Ufa, Nyanda za Chini za Kusini-Mashariki na Ukanda wa Pwani.”

Idara hiyo ilionya kuwa katika baadhi ya maeneo ndani ya kanda hizo, huenda kukashuhudiwa mvua kubwa za hapa na pale, na kuongeza hatari ya mafuriko ya ghafla katika maeneo ya mabondeni na maporomoko ya ardhi katika maeneo ya milimani.

Kadhalika, usafiri unaweza kuvurugika na pia mafuriko ya muda katika miji yanaweza kutokea ikiwa mifumo ya mabomba ya maji itazidiwa.

Ingawa mvua inatarajiwa katika sehemu nyingi za nchi, idara hiyo ilisema baadhi ya maeneo yataendelea kuwa na jua na ukavu katika kipindi cha utabiri.

Baadhi ya maeneo ya Kaskazini-Mashariki na Kaskazini-Magharibi mwa Kenya yanatarajiwa kushuhudia hali kavu kwa kiasi kikubwa, ingawa manyunyu mepesi yanaweza kushuhudiwa katika maeneo machache.

Halijoto ya mchana katika maeneo ya pwani pamoja na Kaskazini-Mashariki na Kaskazini-Magharibi mwa Kenya huenda ikapanda zaidi ya nyuzi joto 30. 

 
“Halijoto ya usiku inatarajiwa kushuka katika baadhi ya maeneo ya nyanda za juu,” utabiri wa hali ya anga uliarifu.