Hali ya ukame katika Kaunti ya Mandera imeendelea kuzorota, huku zaidi ya watu 335,000 wakihitaji msaada wa dharura. 
 
Kati yao, takriban watu 120,000 wanategemea maji yanayosafirishwa kwa malori, hali iliyosababisha kaunti hiyo kuingia katika hatua ya tahadhari kali (Alarm Phase).

Kwa mujibu wa taarifa zilizopo, zaidi ya asilimia 80 ya vyanzo vya maji vimekauka kabisa. Mito, mabwawa na visima ambavyo awali vilikuwa tegemeo la jamii sasa vimebaki tope, ishara ya ukame uliokithiri unaoikumba kaunti hily.

Mifugo, iliyokuwa uti wa mgongo wa maisha ya wakazi, imeonekana kudhoofika na kukosa lishe kutokana na uhaba wa maji na malisho. Katika baadhi ya maeneo, mizoga ya wanyama imetapakaa, ikionyesha kiwango kikubwa cha hasara iliyosababishwa na ukame. Sokoni, bei ya ngamia, mbuzi na ng’ombe imeshuka kutokana na hali yao kiafya.

Chini ya jua kali, akina mama wakiwa wamewabeba watoto mgongoni wanalazimika kutembea umbali mrefu wakiwa na mitungi mikononi kutafuta maji, huku hatima yao ikiwa haijulikani. Inaripotiwa kuwa ngamia, waliokuwa wakitegemea malisho ya asili, sasa wanalishwa chakula cha nyumbani ili kuendelea kuishi.

Katika harakati za kuokoa maisha, wakazi wanalazimika kupanga foleni kwa saa nyingi ili kujaza dumu moja la maji. Kila tone la maji ni ushindi, na kila safari ni hatari, hali inayodhihirisha uzito wa janga la ukame linaloikumba Mandera.

 
“Kaunti zote ndogo katika Kaunti ya Mandera zinakabiliwa na hali mbaya ya ukame, hali iliyoacha familia nyingi zikiwa katika hatari ya uhaba wa chakula na kuhitaji msaada wa dharura,” alisema Waziri wa Utumishi wa Umma, Geoffrey Ruku.

Aliongeza kuwa, kufuatia hali hiyo, “serikali hadi sasa imesambaza jumla ya magunia 26,320 ya mchele yenye kilo 50 kila moja na magunia 14,360 ya maharagwe yenye kilo 50 kila moja katika kaunti ndogo mbalimbali za Mandera, ili kusaidia kuzuia makali ya njaa.”