Shirika la Msalaba Mwekundu Nchini (KRC) linaendelea kutoa tahadhari ya ukame unaoendelea kushuhudiwa sehemu mbalimbali nchini, zaidi ya wakenya milioni mbili wakiwa wameathirika, kaunti 32 zikiwa katika hali hatari.
 
Serikali hata hivyo, imetangaza mipango ya kusambaza nyasi kavu (hay) katika maeneo yaliyoathiriwa zaidi na ukame kama sehemu ya juhudi za kukabiliana na vipindi virefu vya ukame vinavyoendelea kushuhudiwa katika maeneo kame na nusu-kame (ASAL) nchini.

Kwa mujibu wa shirika la kushughulikia majanga – NDMA, jamii za wafugaji zinaendelea kubeba mzigo mkubwa wa athari za mabadiliko ya tabianchi baada ya mvua za vuli zilizotarajiwa kunyesha kati ya Oktoba hadi Desemba mwaka uliopita, kukosa kunyesha katika maeneo mengi ambayo hushuhudia ukame – ASAL. 

 
Kutokana na hali hiyo, NDMA imesema kaunti zipatazo 32 zimeathirika pakubwa na vipindi virefu vya ukame, hali inayotishia maisha na riziki za wafugaji wanaotegemea mifugo.

Kama sehemu ya hatua za kuingilia kati, maafisa wa Shirika la Utafiti wa Kilimo na Mifugo Kenya (KALRO) wakiongozwa na Mkurugenzi Mkuu Dkt. Patrick Kiretien, wamehusishwa kusaidia juhudi za kusambaza chakula cha mifugo katika maeneo yaliyoathiriwa, hatua inayotarajiwa kupunguza hasara zaidi kwa wafugaji, serikali ikitakiwa kuanza kununua mifugo hao ili kuchinjwa kuepukea hasara.

https://twitter.com/KenyaRedCross/status/2016134240258158821

Kadhalika, Shirika la Kitaifa la Msalaba Mwekundu, kwa ushirikiano na wadau wake, unaendelea kusambaza maji, chakula na msaada wa fedha taslimu kwa familia zilizo hatarini ili kuwasaidia kukabiliana na hali inayozidi kuwa mbaya.

Image
 
Kulingana na ripoti za hivi karibuni kuhusu hali ya ukame, kati ya kaunti 32 zilizoathirika, kaunti 11 zimetajwa kuwa katika hali ya hatari kubwa, kaunti ya Baringo (Eneo la Tiaty) na Kaunti ya Mandera zikitambuliwa kuwa katika hali tete zaidi, kwani zinakabiliwa na viwango vya juu vya utapiamlo.

Kwa kuwa utabiri wa hali ya hewa unaonyesha kuwa angalau miezi miwili ijayo itakuwa na mvua kidogo au kutokuwepo kabisa kwa mvua, mamlaka zinaonya kuwa hali ya ukame huenda ikaendelea kuwa mbaya zaidi endapo hatua za dharura hazitaimarishwa.

 
“Serikali inaendelea kutathmini athari za ukame katika maeneo ya Kaskazini mwa Kenya na sehemu nyingine za nchi, huku ikichukua hatua za haraka kuzuia upotevu wa maisha,” alisema Waziri wa Utumisi wa Umma na Mipango Maalum, Geofrey Ruku, Jumatatu.

Wakati mjadala kuhusu siasa za eneo la Kaskazini Mashariki ukiendelea, waziri huyo aliongezea kuwa “kipaumbele cha serikali kwa sasa ni kuandaa na kutekeleza hatua za dharura ili kuhakikisha hakuna Mkenya, kutoka sehemu yoyote ya nchi, anayepoteza maisha kutokana na uhaba wa chakula.” 

Image
 
Ukame wa mara kwa mara katika maeneo kame na nusu-kame umeendelea kuchochea migogoro kutokana na ushindani wa rasilimali adimu kama maji na malisho, hali inayodhoofisha maisha ya jamii na kusababisha ukosefu wa usalama.


Katika ukanda wa Isiolo–Garissa–Meru, changamoto hizi zimechangia uhamaji wa wakazi na mifugo wao, na kudidimiza maendeleo. 

 
Ili kukabiliana na hali hiyo, Mamlaka ya Kitaifa ya Kudhibiti Ukame (NDMA) kwa ushirikiano na serikali za kaunti za Garissa, Isiolo na Meru, pamoja na mashirika ya kijamii, sasa imeandaa Msafara wa Amani kwa Ustahimilivu wa Jamii.

Msafara huo unaoendeshwa chini ya kaulimbiu “Tudhibiti ukame, kwa amani na malisho endelevu,” ukiwa na lengo la kuhamasisha kuishi kwa amani na kuhakikisha mgawanyo wa haki wa rasilimali asilia, unatarajiwa kufanyika kuanzia Februari 2 – 5, 2026.