Serikali ya Afrika Kusini imewakamata raia saba wa Kenya wanaotuhumiwa kufanya kazi nchini humo kinyume cha sheria na bila kuwa na nyaraka na vibali hitajika na wanatarajiwa kurejeshwa nchini.
Wakenya hao ambao waliingia nchini humo kwa viza ya utalii, walikutwa wakifanya kazi ya kuwasajili wale ambao wanaomba hifadhi ya wakimbizi kupitia mpango wa serikali ya Amerika.
Kulingana na mamlaka za Afrika Kusini, Wakenya hao ambao hawakuwa na nyaraka zinazowaruhusu kufanya kazi nchini humo, “waliajiriwa na shirika moja lisilo la serikali nchini Kenya ambalo lilipewa mkataba wa kuwasajili raia Wazungu wa Afrika Kusini wanaotaka kuomba uhifadhi ya nchini Amerika.”
Kukamatwa kwa Wakenya hao Jumanne, Desemba 16, 2025 kulifuatia upelelezi na uvamizi katika kituo kimoja cha kushughulikia maombi ya wakimbizi na walikutwa wakiandaa nyaraka za visa ili waweze kusafiri Amerika kama wakimbizi.
Maafisa wa Afrika Kusini wamesema watu hao hawakukamatwa kwenye eneo la kidiplomasia kama walivyodai maafisa wa Marekani, katika taifa hilo la Rais Cyril Ramaphosa.
Mwezi Oktoba mwaka huu utawala wa Rais wa Marekanii Donald Trump ulitangaza mpango wa kutoa hifadhi za wakimbizi kwa raia Wazungu wa Afrika Kusini maarufu kama ‘Afrikaner’ wapatao 7,500 katika mwaka huu wa kifedha.
Idadi hiyo ni chini ya ile iliyokuwa imepangiwa ya watu 100,000 chini ya utawala wa Rais Joe Biden, na baada ya hapo kundi la watu 50 waliweza kuhamia Marekani chini ya mpango huo.
Tangu wakati huo, vikundi vidogo vidogo vya watu vimekuwa vikiondoka Afrika Kusini chini ya mpango huo kuelekea Marekani.